BANDARI YA MTWARA YAPOKEA WATUMISHI WAPYA
Bandari ya Mtwara imepokea jumla ya watumishi wapya 21 waliowasili rasmi Februari 16, 2026, kwa lengo la kuimarisha rasilimali watu na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma bandarini.
Watumishi hao wametoka katika kada mbalimbali zikiwemo Ubaharia, Ulinzi, Zimamoto na Rasilimaliwatu, hatua inayolenga kuimarisha utendaji kazi katika maeneo muhimu ya uendeshaji wa bandari hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya mapokezi, Afisa Rasilimaliwatu Mkuu, Bw. Mtunze M. Sudi, aliwapongeza watumishi hao kwa kuanza rasmi safari yao ya Utumishi wa Umma. Aliwasisitiza umuhimu wa uwajibikaji, nidhamu na kufanya kazi kwa weledi ili kufikia malengo ya taasisi.
Aidha, aliwahimiza kuzingatia misingi, kanuni na taratibu za kazi zilizowekwa, kufanya kazi kwa ushirikiano na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuathiri maadili ya Utumishi wa Umma. Alieleza kuwa kila mtumishi ana wajibu wa kulinda heshima na hadhi ya taasisi kwa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu na bidii.
Ujio wa watumishi hao unatarajiwa kuongeza tija, kuimarisha utoaji wa huduma kwa wadau mbalimbali na kuendelea kuifanya Bandari ya Mtwara kuwa kitovu muhimu cha biashara katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania pamoja na nchi jirani.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada endelevu za TPA katika kuboresha miundombinu na rasilimali watu, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa kupitia sekta ya bandari.

EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"