BANDARI YA KILWA YA YAPOKEA MELI YA WATALI MV LE BELLOT
Bandari ya Kilwa imeendelea kuwa nguzo kubwa ya kuvutia, kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii Nchini kufuatia kuwasili kwa Meli ya MV LE BELLOT, tarehe 11 Februari, 2026 ikiwa na jumla ya watalii 152 pamoja na wafanyakazi 133.
Ujio wa Meli hiyo unawapa Watalii hao fursa ya kutembelea na kujionea urithi wa kipekee pamoja na vivutio vya kihistoria na kitamaduni vilivyopo Kilwa Kisiwani, eneo lenye umuhimu mkubwa kihistoria.
Watalii hao wanatoka katika Mataifa mbalimbali Duniani ikiwemo Kenya, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Canada, Australia, Uswisi, Hispania, Shelisheli, Norway, Chile na Ubelgiji.
Mchanganyiko huo wa Mataifa unaendelea kuthibitisha hadhi ya Tanzania kama kitovu cha utalii kinachozidi kuvutia Kimataifa. Mafanikio haya yanatokana na juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha na kuboresha Sera, Sheria, Miundombinu, Kuendeleza maeneo ya urithi na Kutangaza vivutio vya Utalii nje ya Nchi.
Aidha, juhudi kubwa zimeendelea kutekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania katika kuboresha huduma na mazingira ya upokeaji wa meli mbalimbali ikiwemo za Utalii, hatua inayochochea hamasa kwa wadau wa sekta hiyo na kufanya Bandari za Tanzania kuwa chaguo la kuaminika.
Ongezeko la ujio wa Meli za Utalii ni ishara ya mafanikio ya mikakati ya Kitaifa ya kukuza Utalii, Kuongeza mapato ya Nchi, kufungua milango ya fursa za ajira na biashara kwa wananchi wa maeneo husika. Tanzania inaendelea kusonga mbele na kuwa kivutio bora cha Utalii Barani Afrika na Duniani kwa ujumla.
EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"