TPA YAPONGEZWA NA MJUMBE WA BODI YA CRDB KWA JUHUDI ZA KUPANUA WIGO WA SOKO NCHINI DRC

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Bw. Charles Carley, ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kwa juhudi madhubuti za kupanua wigo wa soko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hususani kupitia huduma zinazotolewa katika Mkoa wa Lualaba.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 16 Juni 2025, katika ziara rasmi ya ujumbe wa Utawala wa Benki ya CRDB-Congo walipotembelea ofisi ya TPA mkoani Kolwezi, kisha kushiriki mkutano muhimu baina ya TPA, CRDB na Shirikisho la Makampuni ya Biashara Congo (FEC) – Lualaba.
Mkutano huu ni sehemu ya muendelezo wa mashauriano ya kibiashara yaliyoanzishwa kupitia kongamano la wadau lililoandaliwa na TPA mwezi Aprili 2025 chini ya kaulimbiu isemayo “Kwa pamoja tunatengeneza kesho bora si ya TPA na sekta ya biashara ya Lualaba pekee, bali pia mafanikio ya kiuchumi ya Tanzania na DRC kwa ujumla.”
Kwa niaba ya TPA, Afisa Mwakilishi Bi. Kuruthum Ngunguti alieleza umuhimu wa ushirikiano na taasisi za kifedha kama CRDB katika kurahisisha michakato ya malipo ya huduma za bandari, jambo linaloongeza ufanisi na kuimarisha uzoefu wa wateja wa TPA.