Sélectionnez votre langue

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imewasilisha taarifa yake ya Utekelezaji kwa mwaka 2024/25 iliyosheheni taarifa za miradi iliyotekelezwa, inayoanza kutekelezwa na fursa zilizopo za uwekezaji katika Ujenzi na maboresho ya bandari za TPA ili kuongeza ufanisi katika bandari za Tanzania.

 Hayo yameelezwa Disemba 16, 2025 na Mkurugenzi wa Mipango, Ubora na Udhibiti Vihatarishi Dkt. Boniface Nobeji kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Plasduce Mkeli Mbosa wakati akifanya wasilisho katika Mkutano wa 18 wa tathimini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).

Katika wasilisho lake Dkt. Nobeji ametaja miradi mikubwa inayotekelezwa na TPA kuwa ni pamoja ujenzi wa matenki 15 ya kupokelea na kusambaza mafuta yanayojengwa Kigamboni Jijini Dar es salaam, ujenzi wa gati lenye urefu wa mita 500 Malindi Wharf katika Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa Bandari mpya ya Kisiwa Mgao Mkoani Mtwara, ujenzi wa bandari mpya ya Mbamba Bay, katika Ziwa Nyasa na maboresho na upanuzi wa bandari za Bukoba, Kemondo na Mwanza Kaskazini katika ZiwaVictoria.

Aidha Dkt.Nobeji aliitaja miradi iliyokwisha kamilika kuwa ni maboresho ya gati na utanuzi wa lango la kuingialia na kutokea meli, kupanua eneo la kugeuzia Meli katika bandari za Dar es salaam, Tanga na Mtwara.

 Miradi mingine iliyokamilika ni ujenzi wa gati jipya la kuhudumia meli za magari na eneo lake la kuegeshea magari lenye uwezo wa kubeba magari alfu sita (6000) katika bandari ya Dar es salam pamoja na usimikaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA katika bandari ya Dar es salaam, Tanga na Mtwara.

 Miradi inayoendelewa kutekelezwa na inayotarajiwa kuanza ni ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mbegani Bagamoyo na ujenzi wa gati nne za kuhudumia meli za mafuta zenye uwezo wa kuhudumia meli nne za mafuta kwa wakati mmoja katika eneo la Kendwa Kigamboni.

Aidha, Dkt. Nobeji alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka sekta binafsi kushiriki kwa pamoja na Serikali kupitia TPA kujenga na kuendesha bandari ili kuhakikisha kwamba, miradi hiyo ya kimkakati inatekelezwa kwa wakati.