Sélectionnez votre langue

Bandari ya Dar es Salaam imevuka lengo la utendaji kwa kuhudumia jumla ya Tani Milioni 27.7 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 tofauti ya lengo lililowekwa la kuhudumia Tani Milioni 25.

Mafanikio hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed G. Abed, tarehe 23 Julai 2025 wakati akifungua Kikao cha Tatu (3) cha Baraza la Majadiliano kituo cha Bandari ya Dar es Salaam kilichofanyika mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

“Ninawapongeza sana kwa ufanisi bora kwa mwaka fedha 2024/2025 tumevuka lengo kwa Tani Milioni 2.7 pia tupo mbele ya ufanisi wa jumla ya Tani Milioni 23.69 kwa Mwaka wa fedha 2023/2024, “ alisema Bw. Abed. 

Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja ushirikiano wa watendaji wa TPA, wadau mbalimbali na Vyombo vya Usalama waliowezesha shehena kusafirishwa kwa urahisi.

Aidha Bw.Abed amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari Tanzania (DOWUTA) ambao wamewezesha kudumisha amani na utulivu katika Bandari ya Dar es Salaam.