Sélectionnez votre langue

Bandari ya Tanga mevunja rekodi katika kuhudumia meli, shehena na ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha robo mwaka cha Julai - Septemba  2025.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Bandari ya Tanga, Bw. Salehe Mbega wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma Kwa Wateja ambayo uadhimishwa Mwezi Oktoba ya kila Mwaka.

Mbega amesema katika kipindi cha robo mwaka Julai - Septemba 2025 Bandari ya Tanga imehudumia meli 52 za bahari ya mbali (deep sea) wakati lengo lilikuwa kuhudumia meli 37 sawa na ongezeko la asilimia 40.5. 

Aidha, idadi ya hiyo ya meli zilizohudumiwa kwa kipindi hicho ni zaidi kwa asilimia 30 au meli 12 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha Julai - Septemba 2024 ambapo idadi ya meli zilizohudumiwa zilikua 40

Pia Meneja huyo amesema kwa upande wa shehena ya mzigo kwa kipindi cha Julai - Septemba 2025 bandari imehudumia tani 508,373 wakati lengo lilikuwa kuhudumia tani 413,591 sawa na ongezeko la asilimia 22.9 ya lengo. 

Aidha kiasi hicho cha shehena kilichohudumiwa kilikua ni zaidi kwa tani 174,730 au asilimia 52.37 kikilinganishwa na kipindi kama hicho cha Julai - Septemba 2024 ambapo bandari ilihudumia tani 333,643.

Halikadhalika, kwa upande wa mapato Mbega amesema katika kipindi cha Julai - Septemba 2025 Bandari ya Tanga imekusanya jumla ya Shilingi 
 Bilioni 31.671 wakati lengo lilikuwa ni kukusanya Shilingi Bilioni 21.350 sawa na ongezeko la asilimia 48.34. 

Vievile, kiasi hicho cha mapato kilichokusanywa kilikua ni zaidi kwa Shilingi 13.040 bilioni sawa na asilimia 69.98 Ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha Julai - Septemba 2024 ambapo Bandari ilikusanya Shilingi Bilioni 18.631.

Wakati Bandari ya Tanga inaungana na taasisi na makampuni kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, Meneja wa Bandari Bw. Salehe Mbega, amewashukuru na kuwapongeza wadau na wateja kwani wamekuwa sehemu ya mafanikio hayo ya kuvunja rekodi katika utendaji  na ongezeko la tija kwa Bandari ya Tanga kwani bila wateja na wadau bandari isingeweza kupata mafanikio hayo.

Bw. Mbega amewahidi wateja na wadau wa bandari kwamba, Bandari ya Tanga imejipanga kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake. "Tukiwa tunaadhimisha wiki ya huduma kwa wateja sisi kama Bandari ya Tanga  tumejipanga kuendelea kutoa huduma iliyobora ya viwango vya Kimataifa ili tuzidi kuvutia wateja wengi zaidi kutumia bandari yetu ambayo imeboresha huduma zake”. Aliongeza Bw. Mbega 

Aidha wateja na wadau waliipongeza Bandari ya Tanga kwa kutoa huduma bora kwa wateja wake kwa muda wa saa 24 katika siku 7 za wiki. Wateja hao wamewasihi wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili waendelee kuitumia Bandari ya Tanga.