BANDARI YA MTWARA KUANZA KUPOKEA MELI ZENYE SHEHENA ZA MAFUTA
Bandari ya Mtwara imeanza rasmi kupokea na kuhudumia meli zenye shehena za mafuta yanayosafirishwa kwenda Nchi jirani za Zambia na Malawi ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha biashara na usafirishaji wa bidhaa.
Akiongea Oktoba 08,2025 wakati wa hafla ya mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi amesema, huduma hiyo imeanza kutolewa tangu mwezi Septemba na kuendelea mwezi huu wa Oktoba ambapo ujio wa meli hizo ni ishara ya maendeleo makubwa katika Bandari ya Mtwara kwa kuwa awali haikuhudumia shehena za mafuta kwa ajili ya nchi hizo jirani.
Ameongeza kuwa, kasi ya usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Mtwara imeongezeka kwa kiwango kikubwa ambapo kwa sasa inahudumia zaidi ya tani milioni 2.5 kwa mwaka 2024/2025 ikilinganishwa na tani 500,000 kwa mwaka 2021/2022.
Kwa upande wa baadhi ya wadau wa Bandari walioshiriki hafla hiyo, wamepongeza maboresho yaliyofanyika kwenye miundombinu na vifaa ambapo huduma zimeimarika kwa kiwango kikubwa. Wamepongeza pia uongozi wa Bandari kwa kuendelea kushirikiana na wadau katika kuboresha huduma.


EN
SW
FR
TPA ChatBot - "Nahodha"