Sélectionnez votre langue

AZIRI wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ( Mb), amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan haijajielekeza kujenga miundombinu pekee, bali kuhakikisha Bandari mpya ya Mbamba Bay inakuwa kitovu cha biashara, usafirishaji na uchumi katika ukanda wa Ziwa Nyasa, hatua itakayofungua masoko mapya kwa wakulima, wavuvi, wafanyabiashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania ndani na nje ya nchi. Mhe. Prof. Mbarawa ameyasema hayo, Julai 11, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari mpya ya Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza na wananchi wa Mbamba Bay, viongozi wa Serikali na wataalamu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), amesema uwekezaji wa Serikali wa shilingi bilioni 80.56 katika mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kupitia uboreshaji wa miundombinu ya usafiri wa majini katika Maziwa Makuu. Amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo uliofikisha asilimia 60, kiwango ambacho kinaonyesha maendeleo makubwa ikilinganishwa na alipotembelea eneo hilo mwezi Januari mwaka huu.

Mapema, akimkaribisha Waziri Prof. Mbarawa, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kupeleka miradi mikubwa ya maendeleo mkoani humo, akisema Bandari ya Mbamba Bay itakuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Wilaya ya Nyasa na maeneo ya jirani kutokana na nafasi yake kama lango muhimu la uchumi wa Ziwa Nyasa. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi kutoka TPA, Mhandisi Erick Madinda, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, amesema mradi huo umefikia asilimia 60 ya utekelezaji na unaendelea kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu, usalama na utunzaji wa mazingira. Amesema kukamilika kwa Bandari ya Mbamba Bay kutaimarisha biashara kati ya Tanzania, Malawi na Msumbiji, pamoja na kuongeza ufanisi wa usafiri wa majini katika ukanda wa Ziwa Nyasa.