TPA imekabidhi jumla ya vitanda saba (7) vya kujifungulia akina mama pamoja na vyandarua mia tatu (300) kwa hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Musoma iliyopo Mkoa wa Mara. Hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa tiba hivyo vyenye thamani ya Sh. Milioni 15 imefanyika Jumatatu Oktoba 02, 2017 hospitalini hapo ambapo mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA alivikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma. Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Naibu Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Lazaro Twange amesema msaada huo ambao umetolewa na TPA ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kuboresha sekta ya huduma za afya. Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dk. Vincent Naano ameishukuru TPA kwa kuacha shughuli zake nyingine muhimu na kuamua kutoa msaada huo mkubwa kwa Mkoa wa Mara. “Msaada huu hautatumika kwa hospitali kuu tu bali utasambazwa kwa vituo vingine vya afya vya bweri, nyasho, mwangi na nyamatare ambako utasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaofika hospitali kuu kwa kukosa huduma vituoni” amesema Dk. Naano. Ameongeza kwamba Wilaya ya Musoma inashirikiana kwa karibu na Mamlaka mbalimbali katika kuwaletea Wananchi wake maendeleo na kukumbusha kwamba mwaka juzi (2015) TPA iliisaidia Wilaya yake kwenye ununuzi wa madawati na sasa imesaidia sekta ya afya na kuwaasa wadau wengine kujitokeza kusaidia hasa katika ujenzi wa madarasa ambao kuna upungufu mkubwa. Sera ya TPA ya misaada kwa jamii inalenga katika kuchangia huduma za Afya, Elimu na Maendeleo ya Jamii ambapo katika kipindi cha mwaka 2016/2017, yatari Mamlaka imetoa msaada wenye thamani ya Shilingi Milioni 75 kwa bandari zilizopo kwenye Ziwa Victoria pekee.