UPANUZI WA BANDARI YA TANGA KUSAIDIA WATANZANIA KUACHA KUTUMIA BANDARI YA MOMBASA NCHINI KENYA.

Wadau wa bandari nchini wamesema uwekezaji wa shilingi bilioni 429 kwenye bandari ya Tanga kwa ajili ya ujenzi wa gati mbili za kisasa katika bandari ya Tanga utasaidia watanzania kuacha kutumia bandari ya Mombasa nchini Kenya.

Lakini pia uwekezaji uliofanywa na serikali katika bandari ya Tanga, utaisaidia kuongeza mapato baada ya meli kubwa kufika kushusha mizigo.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea bandari hiyo, wadau wanaohudhuria mkutano unaojadili changamoto zinazoikumba bandari hapa nchini, walisema kuwa upanuzi wa gati katika bandari ya Tanga kutasababisha waweze kuhudumia meli kubwa.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Wakala wa Meli nchini (TASAA) Daniel Malango alisema mabadiliko yaliyofanyika yanaleta suluhisho la meli zilizokuwa zikishushia mizigo nchi jirani ya Kenya, zitafika katika banadari hiyo.

“Tulichokiona Tanga tunaweza kusema ni ‘game changer’ kwamba kuna uwekezaji serikali imefanya, sasa naiona Tanga inakuwa suluhisho la mizigo iliyokuwa inapitia Mombasa, Meli kubwa zitafika hapa na Revenue zetu zitakuwa juu,” alisema Bw Malango.

Alisema matayarisho yaliyofanywa kwa ajili ya kontena na mizigo mingine ambayo itasaidia kukuza uchumi kwa kuwa mapati yatapanda.

Naye ofisa sera, mazingira wa shirikisho la viwanda nchini (CTI) Anna Kimaro alisema kwa maboresho yaliyofanywa na serikali yataleta fursa kwa wadau wanaosafirisha mizigo kwenda nchi mbalimbali baada ya meli kubwa kufika bandari hiyo.

Alisema pia itaisaidia kupunguza msongamano na mlundikano wa mizigo katika bandari ya Dar es salaam na hivyo kuisaidia serikali kupata mapato.

Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Aron Kisaka alisema mradi wa maboresho ya bandari katika kuhudumia mizigo hadi kufikia tani milioni tatu unaofanywa katika bandari hiyo utasaidia kufikia kina cha mita 13.

Alisema mradi huo ukikamilika utasaidia kupunguza mizigo inayohudumiwa katika bandari ya Dar es salaam hasa kwa wakazi wa mikoa ya Kaskazini na kwasasa watatumia muda mfupi kupitia bandari ya Tanga.

Awali meneja wa bandari ya Tanga, mhandisi Masoud Mrisha alisema mradi huo ambao upo awamu ya pili ya utekelezwaji wake umfikia asilimia 45 na utarajiwa kukabidhiwa Novemba mwaka huu utakaokuwa na mita 450.

Alisema mradi huo ukikamilika utaweza kuhudumia kiasi cha tanimilioni 3 ambapo kwa sasa bandari hiyo inauwezo wa kuhudumia tani laki saba tu.

Kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuhudumia tani milioni tatu ambapo kwa sasa bandari hiyo inahudumia tani laki saba na hamsini kwa mwaka.