Mkurugenzi Mpya wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Mrisho S. Mrisho

Na Levina Msia

Mkurugenzi Mpya wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Mrisho S. Mrisho amefungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Bandari ya Dar ea Salaam na kubainisha vipaumbele vyake ili kuongeza ufanisi.

Katika kikao hicho ambacho ni cha kwanza tangu ateuliwe kushika nafasi ya Ukurugenzi wa Bandari hiyo, Mkurugenzi huyo alibainisha vipaumbele vyake vinavyolenga kuongeza ufanisi katika utendaji bandarini hapo.

Miongoni mwa vipaumbele alivyoainisha kuvisimamia kwa haraka ni pamoja na kuongeza kasi ya upatikanaji wa vitendea kazi, uboreshaji wa maeneo ya utendaji kazi, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya ofisi na maeneo mbalimbali ya shughuli za utekelezaji.

vingine ni pamoja na kuisafisha Bandari kwa kupanga vyema yadi za kuhifadhia shehena,  kuvuka malengo ya kiutendaji, kutoa motisha kwa wafanyakazi wanaofanya vizuri, kuimarisha kitengo cha ‘welfare’ ili kukabiliana na matatizo ya ndani ya wafanyakazi, kusimamia kwa karibu michakato ya manunuzi kwa lengo la kufanikisha upatikanaji wa mahitaji muhimu kama vile vipuri na uboreshaji wa Viwanja vya Michezo.

Wajumbe wa Baraza wameahidi kumpatia ushirikiano Mkurugenzi wa Bandari na kumhakikishia kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya Taasisi na Serikali kwa ujumla.

Mwisho