Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imejipanga kuhudumia shehena ya mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda pindi uzalishaji wa bidhaa hiyo utakapoanza rasmi mwaka 2025. Tanzania ilishinda tenda ya kupitisha mafuta ghafi kwa njia ya bomba kutoka mji wa Hoima yanapozalishwa hadi kwenye masoko ya nje kupitia Bandari ya Chongoleani mjni Tanga . Uamuzi wa Mwisho wa Uwekezaji wa miradi ya juu na EACOP ulitangazwa tarehe 1 Februari, 2022 na maendeleo ya mradi yanaendelea kwa lengo la Mafuta ya Kwanza mwaka 2025. Haya yalisemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano, Dkt. George Fasha wakati wa mkutano na maonyesho ya 10 wa Mafuta ya Afika Mashariki uliofanyika Nchini Uganda. Dkt Fasha ambaye alikuwa ni mmoja wa wasilishaji mada katika mkutano huo, alisema TPA kupitia Bandari yake ya Chongoleani iliyopo mjini Tanga, imejipanga kuhudumia shehena hiyo kwa ufanisi mkubwa. Amesema kwamba Bandari ni Lango la Biashara, Kitaifa na Kimataifa, hivyo kama ikitumiwa ipasanvyo itafungua milango ya biashara na maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za Afrika Mashariki. “Ili kufanikisha haya, tuna mradi mkubwa wa kimkakati unaojulikana kama DMGP ambao umejikita katika kufanya maboresho ya kimiundombinu kwa Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Dkt. Fasha. Mradi huu unahusisha pamoja na mambo mengine, maboresho ya kiutendaji kwa wafanyakazi wetu ambao wamepatiwa mafunzo mablimbali ya jinsi ya kuhudumia meli na mizigo inayopita Bandari ya Dar es Salaam na zinginezo. Mkutano huo uliolenga kuionyesha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama kimbilio la chaguo la fursa za uwekezaji wa mafuta na gesi ili kuboresha mageuzi ya kijamii na kiuchumi. Bandari ni lango la biashara na kama ikitumiwa ipasanvyo itafungua mialngo la biashara na maendeleo ya kiuchumi. Ili kufanikisha haya, tuna mradi mkubwa wa kimkakati ujulikano kama DMGP ambao lengo lake ni kufanye maboresho ya kimiundombinu kwa Bandari ya DSM Mradi huu unahusisha Pamoja na mambo mengine pia na maboreho ya kiutendaji wa wafanyakazi wetu ambapo wamewezeshwa kwa kupata mafunzo mablimbali ya jinsi ya kuhdumia meli na mzigo inayopita Bandarini. Mwisho
Mwandishi Wetu Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeeleza kuridhishwa kwake na utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam. Akizungumza na mwandishi wa TOVUTI ya TPA, Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye pia ndiye Gavana wa Benki hiyo Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Bodi yake imeridhishwa na utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam hususani mchango wake Katika ukuaji wa uchumi wa nchi. Gavana Tutuba amesema kwamba Bodi yake pia imejiridhisha kuwa Bandari za TPA kupitia uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali, zinaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa fedha za kigeni nchini kupitia mapato yatokanayo na Bandari. “Mapato mengi yanakusanywa kupitia shughuli za kibandari na hapa tumejionea wenyewe utendaji kazi wa Bandari hii na kazi nzuri inayofanyika hapa kulingana na majukumu yetu ya msingi ambayo ni kusimamia masuala ya uchumi, amesema Gavana Tutuba na kuongeza kwamba, tumejadiliana kwa kina na kuangalia namna ambavyo Bandari inavyoweza kuchangia zaidi kwenye ukuaji wa uchumi hasa kupitia upokeaji wa mizigo kutoka nje na kuiondosha kwa haraka kuipeleka kwenye maeneo husika.” Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Balozi na IGP Mstaafu Ernest Mangu, amesema ziara hiyo imekuwa na tija kwa TPA hasa kupitia ushauri uliotolewa kwa TPA juu ya namna bora zaidi ya kuongeza mapato kupitia Bandari zilizopo hapa nchini na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa nchi. “Kuna maeneo ambayo Bodi ya BOT wametupa ushauri na tumeuchukua, na tutautekeleza Kwani lengo kuu ni kuboresha utendaji wetu na kuongeza mapato na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi,” alimesema Balozi Mangu. Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya BOT, Gavana Tutuba aliongozana na Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha wa BOT Bi. Sauda Kassim Msemo na Wajumbe wa Bodi yake huku kwa Upande wa TPA mbali na Mwenyekiti wa Bodi Balozi Ernest Mangu, alikuwepo pia Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, Mkurugenzi wa Bandari ya DSM, Bw. Mrisho Mrisho pamoja na wajumbe wengine wa Menejimenti ya TPA. Mwisho
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania - TPA, tarehe 10 Mei, 2023 imewakutanisha Wadau wa shughuli za Bandari Nchini katika Semina ya kujenga uelewa kuhusu Mradi wa Upanuzi na Maboresho ya Miundombinu ya Bandari ya DSM. Mradi huo unahusisha ujenzi wa Gati maalum ya kuhudumia Meli kubwa za Kitalii, Kuboresha Miundombinu ya Gati la kuhudumia Abiria na Mizigo kwa Meli za Mwambao na Ujenzi wa Gati mpya nne za kuhudumia Makasha ( Makontena) Katika Bandari ya Dar es Salaam. Akizungumza katika Semina hiyo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA Bw. Ntandu Mathayo amesema Mradi huo utakapokamilika, utaongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhudumia Shehena kutoka tani milioni 17 kufikia tani Milioni 28 kwa mwaka
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Atupele Mwakibete amekagua maendeleo ya ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala ili kuona kama ipo tayari kuanza kutoa huduma. Kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa bandari hiyo, kutaongeza ufanisi na kuchochea kukua zaidi kwa shehena inayohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam. Mbali ya kuchochea ukuaji wa shehena na kuongeza ufanisi, kukamilika kwa bandari hiyo pia kutasaidia kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza mapato ya Serikali kupitia huduma zitakazokuwa zikitolewa bandarini hapo. Kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Kwala ni matokeo chanya ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan ambayo imewezesha ujenzi huo kwa kuidhinisha kiasi cha TZS 83.247 Bilioni kutumika kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo. Mradi wa Bandari hiyo unahusisha ujenzi wa Barabara ya zege yenye urefu wa Kilometa 15.5 kutoka Mzani wa Vigwaza hadi kuingia Bandarini pamoja na ujenzi wa miundombinu ya reli mchepuko yenye urefu wa kilometa 1.3
Ujumbe wa Maofisa wa Forodha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Forodha na Ushuru wa bidhaa Bw. René Kalala Masimango, umeipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania - TPA kwa kuweka mikakati madhubuti ya ujenzi na uimarishwaji wa Bandari Kavu ya Kwala iliyopo Mkoa wa Pwani. Bw. Masimango anayesimamia Majimbo ya Haut Katanga, Lualaba, Tanganyika na Lomami ametoa pongezi hizo tarehe 05 Mei,2023 alipotembelea Bandari Kavu ya Kwala ili kujionea utayari wa Bandari hiyo katika kutoa huduma. “Tunawapongeza kwa kazi nzuri. Majimbo ninayoyasimamia, Jimbo la Haut Katanga linapokea asilimia 80 ya Shehena ya DRC inayopitia Bandari ya Dar es Salaam, hivyo ni muhimu sana kwetu kufika hapa katika Bandari Kavu ya Kwala ili kujionea utayari wale kwa ajili ya kuhudumia shehena zetu”, amesema Bw. Masimango. Naye Balozi wa Tanzania nchini DRC Mhe. Said Juma Mshana amesema lengo la ziara hii ya Kibiashara ni kuona utendaji kazi wa Bandari ya Dar es Salaam na hii ya Kwala ili kuimarisha Biashara Kati ya Tanzania na DRC. “Tupo hapa kurahisisha Biashara, uwekezaji na kutanua masoko kati ya nchi hizi mbili za Tanzania na DRC na hii yote ni katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi,” amesema Mhe. Balozi Mshana. Ujumbe huo ukiwa katika Bandari Kavu ya Kwala, pia umetembelea na kukagua eneo la Hekta 10 lililotengwa na Serikali kwa ajili ya kuhudumia Shehena ya mzigo wa DRC unaopita Katika Bandari ya Dar es Salaam. Ujumbe huo na umepewa maelezo ya kina kuhusu mradi huo na Meneja miliki wa TPA Bw. Alexander Ndibalema ambaye amesema kukamilika na kuanza kutoa huduma kwa Bandari hiyo kutapunguza msongamano Katika Bandari ya Dar es Salaam kwa Asilimia 30 na kuongeza mapato ya Serikali kupitia huduma zinazotolewa Katika Bandari. Kukamilika kwa Bandari kavu hiyo ya Kwala iliyofikia Asilimia 95 ya ujenzi wake, ni matokeo chanya ya uongozi madhubuti ya Serikali ya awamu ya sita ambayo imewezesha Shilingi Bilioni 83.247 kwa ajili ya kujenga na kuendeleza Bandari hiyo, ikuhusisha pia Ujenzi wa Barabara ya Zege yenye urefu wa kilometa 15.5 kutoka Barabara ya Morogoro kuingia na kutoka Bandarini hapo pamoja na miundombinu ya reli mchepuko yenye urefu wa kilometa 1.3 ambayo pia inayoingia na kutoka katika Bandari hiyo. Mwisho
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ( Sekta ya Uchukuzi), Mhe. Atupele Mwakibete, ametembelea na kukagua mradi wa kimkakati wa Maboresho ya Bandari ya Tanga ambao umefikia asilimia 98.9 kukamilika. Mhe. Mwakibete ameridhishwa na kasi ya kukamilishwa kwa Mradi huo kwa wakati na kutoa maelekezo ya kuihuisha haraka iwezekanavyo miundombinu ya Reli inayoingia na kutoka Bandarini hapo ili ianze kufanya kazi haraka.
Na Leonard Magomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imeibuka kinara wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwenye Sekta za Umma na hivyo kukabidhiwa tuzo. Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi. Maonyesho hayo ambayo kwa mwaka huu yalienda na kaulimbiu "Mazingira Salama na yenye Afya Kazini ni Kanuni na Haki ya msingi mahali Pa kazi," yalifanyika katika viwanja vya Tumbaku mjini Morogoro. Wakati wa kilele cha maadhimisho hayo,Prof. Ndalichako alisema kwamba Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia masuala ya usalama na afya mahala pa kazi kwa kuwa ni haki ya msingi wa kila mfanyakazi nchini. Kwa upande mwingine, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na wenye enye ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi alitembelea mabanda yote wakati wa maonyesho hayo. Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na wenye enye ulemavu Patrobas Katambi alipotembelea Banda la TPA wakati wa maonyesho hayo. Sharifu Selemani Jirani Occupational Safety Officer, TPA akipokea tuzo hiyo toka kwa Waziri Ndalichako. Afisa Mwandamizi wa Uhusiano wa TPA, Bw. Leonard Magomba akionyeha tuzo waliyotunukiwa TPA katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi. Baadhi ya wafanyakazi wa TPA wakiwa katika maonyesho hayo Baadhi ya maofisa wa TPA Mwisho
Na Mwandishi Wetu Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC Mhe. Théo Ngwabidje Kasi, ametoa Rai kwa Wawekezaji na Wafanyabiashara wa DRC na Tanzania kuzitumia vema fursa zilizopo kati ya nchi hizo kuimarisha na kuongeza uwekezaji na Biashara zao. Gavana Kasi ametoa Rai hiyo tarehe 29 Aprili, 2023 wakati akifungua kongamano la Uwekezaji na Biashara Mjini Bukavu ambapo amesema Wakuu wa nchi hizi mbili wameweka dhamira ya dhati pamoja na mambo mengine kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kuimarisha Uwekezaji, Biashara na Masoko, hivyo ni vema Wananchi wa nchi zote mbili wakatumia fursa hiyo. " Biashara ni kwa maendeleo ya Nchi zetu na Biashara nyingi inatoka Tanzania kuja Kongo na kutoka huku kwenda Tanzania, hali ya usalama ipo vizuri na hivyo kurahisisha Biashara na usafirishaji Kati ya nchi hizi mbili". Amesema Gavana Kasi. Naye Balozi wa Tanzania Nchini DRC Mhe. Saidi Juma Mshana amesema kufanyika kwa kongamano hilo ni Katika kutekeleza maagizo na maelekezo ya MaRais wa nchi hizi mbili kuhusu Tume ya pamoja ya kudumu ya ushirikiano kwa lengo la kudumisha na kuimarisha uhusiano, ushirikiano na kuboresha miundombinu ikiwemo Bandari , Reli na Barabara ili kurahisisha Biashara na Masoko Kati ya nchi hizi. " Ni muhimu kwa nchi zetu hizi kuendelea kushirikiana na kwa Wafanyabiahara fursa zilizopo zitumike kwa ajili ya manufaa ya nchi zote mbili ikiwemo uwepo wa Bandari ili kurahisisha Biashara na masoko " . Amesema Mhe. Balozi Mshana. Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Dkt. Jilly Maleko amesema Kongamano hili litumike kuimarisha mahusiano na Diplomasia ya kiuchumi na hivyo kukuza Biashara Kati ya nchi hizi mbili. "Nimekuja kutoka Burundi kushiriki nanyi Katika kongamano hili kwa sababu ya Shehena kubwa inayokuja Jimbo la Kivu kusini kutoka Tanzania inapitia Katika nchi ya Burundi, sasa changamoto zote zinazowakabili ni wajibu wa Balozi kuzifanyia kazi ili kurahisisha mazingira ya biashara na kukuza biashara hizo " Amesema Mhe. Balozi Dkt. Maleko. Katika kongamano hilo Mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania -TPA imeshiriki vema ambapo Wawakilishi wake Katika nchi za DRC na Burundi wamewasilisha mada kuhusu thamani na umuhimu wa kutumia Bandari za Tanzania kusafirisha Shehena kufuatia maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali Katika Bandari Nchini na nafuu kubwa ya tozo za Bandari inayotolewa kwa Wasafirishaji wa Shehena wa DRC. Ushiriki wa TPA Katika kongamano hili ulikusudia kukutana na Wasafirishaji wa Bidhaa kwa njia ya maji wa Jimbo la Kivu Kusini na kupata maoni yao kuhusu huduma za Bandari zitolewazo na TPA. Kongamano hilo la siku moja limeshirikisha Serikali ya Jimbo la Kivu kusini- DRC, Balozi za Tanzania nchini DRC na Burundi, TPA , CRDB Burundi na Chemba ya wenye Viwanda, Biashara na Kilimo- TCCIA Mkoa wa Kagera pamoja na Shirikisho la Wafanyabiashara wa Kongo - FEC. Kongamano hilo limelenga kutafuta masoko ya huduma za Taasisi za Tanzania pamoja na masoko ya bidhaa za viwandani na Mazao ya kilimo ya Tanzania Nchini DRC. Mwisho

Subcategories