Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imepokea jumla ya mitambo mipya na ya kisasa 98 kwa ajili ya kupakua na kupakia mizigo Bandarini ili kuongeza kasi na ufanisi. Upatikanaji wa mitambo hiyo ambayo itasambazwa katika Bandari zote nchini, umelenga kuboresha utendaji kazi wa Bandari na kuongeza kasi ya upakiaji na upakuaji wa mizigo inayohudumiwa na Bandari zetu nchini. Akizungumza mara baada ya kupokea mitambo hiyo yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 12.76, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bwana Plasduce Mkeli Mbossa amesema mitambo hiyo yenye ukubwa wa aina tofauti, ina uwezo wa kunyanyua Shehena zenye uzito mbalimbali. “Mitambo hii aina ya ‘Folkal Lift’ imekuja wakati muafaka kwani itasaidia sana katika kuongeza ufanisi katika Bandari zetu,” amesema Mbossa. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Bwana Mrisho S. Mrisho amesema kununuliwa kwa mitambo hiyo mipya ni jambo la faraja mno kwao. “Mitambo hii imekuja wakati muafaka kwani huu ni msimu wa kuhudumia Shehena mbalimbali ikiwemo mazao kwa kiwango kikubwa ambapo mzigo unaingia kutoka mataifa mbalimbali na mazao kusafirishwa kwenda Masoko ya kimataifa,” amesema Mrisho. Mitambo hiyo mipya aina ya “Folkal Lift” itatumika katika Bandari zote nchini zinazosimamiwa na kuendeshwa na TPA. Mwisho